Home » , » HIZI NDIO KANUNI ZINAZOWEZA KUFANYA MAISHA YAKO KUWA MAREFU NA BORA.

HIZI NDIO KANUNI ZINAZOWEZA KUFANYA MAISHA YAKO KUWA MAREFU NA BORA.


HIZI NDIO KANUNI ZINAZOWEZA KUFANYA  MAISHA YAKO KUWA MAREFU NA BORA.
Kwa Tanzania, inakadiriwa kuwa umri wa kuishi kwa wanaume ni takriban miaka 58.2 na kwa wanawake ni miaka 60.5. Muda huu wa kuishi ni mfupi sana ikilinganishwa na wenzetu katika nchi zilizoendelea kama vile Marekani ambako wastani wa kuishi  unakadiriwa kuwa ni miaka 78.2. Hapa ndipo tunapopatwa na maswali mengi kufuatia takwimu hizi tukilinganisha Tanzania na nchi zinazoendelea kama vile Marekani na nchi zinginezo. Wengine husema kuwa tunazeeka na kufa haraka kutokana na kuwa na mtindo usiofaa wa maisha na wengine husema kuwa tunazeeka na kufa mapema kutokana na sababu za maumbile na vinasaba tunavyorithi kwa wazazi wetu.

Tafiti nyingi zinaonyesha kuwa wakazi wa maeneo wanaoishi maisha marefu zaidi duniani kama vile Japani, Italia na Marekani  wanajiepusha na matumizi ya vileo, tumbaku na kupunguza ulaji wa nyama nyekundu. Pia huvuta hewa safi ya kutosha na kupata mapumziko ya kutosha baada ya kazi ngumu kila siku.Watu hawa pia huwa na mtazamo chanya wa maisha, mazoezi na chakula asilia cha mimea kama vile mbogamboga na matunda kwa wingi. 

 KUPUNGUZA ULAJI WA NYAMA NYEKUNDU.
 Ulaji wa nyama nyekundu ni moja ya sababu inayoweza kufanya maisha yako kuwa mafupi kutokana na kuchangia kutokea kwa magonjwa ya moyo, kiharusi, kisukari na saratani ya utumbo. Nyama yenye shida kubwa ni ile yenye mafuta mengi, nyama choma iliyoungua na ile iliyosindikwa. Hii inasababishwa na uzalishaji wa kemikali kama n-nitrosa na polycyclic aromatic hydrocarbons (PAHs) zinazodhuru afya. 

Ingawa jamii ya Wamasai wanakula nyama nyekundu kwa wingi, tafiti zinaonyesha kuwa wanatumia pia mitishamba (acacia goetzei na albizia anthelmintica) kwa wingi. Pia hutumia vyakula vya mimea kwa wingi vikiwa katika uasilia wake, jambo ambalo huwapunguzia hatari itokanayo na nyama. kwa mfano Katika utafiti mmoja uliofanyika huko Japan, wanawake vikongwe 200 walioshiriki katika utafiti walithibitika kuwa katika kipindi cha juma moja, hutumia zaidi ya aina 100 za vyakula vyenye asili ya mimea.

UFANYAJI WA MAZOEZI.
 Katika utafiti mwingine uliofanywa na Dk Dean Ornish na madaktari wenzake wa Chuo Kikuu cha Califonia na San Francisco (UCSF), iligundulika kuwa mazoezi na mtindo bora wa maisha huimarisha afya ya vinasaba vya mwili vinavyohusika na kuzeeka vijulikanavyo kama telomeres. Mazoezi yanaelezewa kuwa hufanya telomeres virefuke, hivyo kuongeza maisha. Telomeres zinapoathirika na kuwa fupi husababisha seli za mwili kudhurika na maisha kuwa mafupi.

UHUSIANO MZURI KATIKA FAMILIA NA JAMII.
Jambo jingine linalochangia kuwa na maisha marefu, ni uhusiano mzuri katika familia na jamii, kwa mujibu wa utafiti wa Rikke Lund wa Chuo Kikuu cha Copenhagen Denmark na wenzake katika jarida la Epidemiolojia na afya ya jamii mwaka 2014. Katika utafiti mwingine uliochapishwa katika jarida la tiba la Uingereza la British Medical, watafiti pia waligundua kuwa kutoelewana, ugomvi na mabishano ya mara kwa mara ya wanafamilia au wanandoa, huchangia watu kufa mapema zaidi. (Mwananchi, Mei 23)


Share this article :